Kasoro katika mchakato utunzi mitihani, mitaala.
UTAFITI wa kitaalamu umeonyesha kuwapo kwa kasoro katika
mchakato wa utunzi wa mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na kubainisha kuwa,
kufeli kwa wanafunzi wa shule za sekondari kunatokana na walimu kutopewa
mafunzo ya utekelezaji wa mitalaa.
Miongoni mwa kasoro zilizobainishwa ni pamoja na utata
kuhusu nafasi za alama za mazoezi katika mtihani wa mwisho na ushiriki wa
walimu na wakuzaji mitalaa katika utunzi wa mitihani hiyo.
Kadhalika matokeo ya utafiti huo ulioratibiwa na Shirika la
HakiElimu, yanaitaja kasoro nyingine kuwa,ni baadhi ya mada za masomo kutungiwa
maswali mengi, huku mada nyingine zikiachwa bila kutungiwa maswali kwa muda
mrefu.
Hata hivyo, utafiti huo umeweka bayana kuwa, hakuna uhusiano
wa moja kwa moja unaothibitisha kuwa mitihani inayotungwa ndio sababu ya
wanafunzi kufeli, kwani kwa kiasi kikubwa maswali yanayotungwa yamekuwa
yakiakisi kilichomo kwenye mitalaa
.
Akiwasilisha ripoti ya utafiti huo kwa wanahabari na wadau
wa elimu jana, Mkuu wa Kitivo cha Elimu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu, Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE), Dk Kitila Mkumbo alisema kuwa, tatizo
lililopo ni walimu kutopatiwa mafunzo ya mitalaa, hasa inapofanyiwa uboreshaji
na kuwapo kwa mazingira duni ya kufundishia na kujifunzia.
“Kuna ongezeko la wanafunzi kufeli mitihani yao ya mwisho na
mara nyingi tumekuwa tukihusisha na sababu nyingine bila kuangalia ushiriki wa
walimu katika uboreshaji wa mitaala,” alisema.
Alisema zaidi ya asilimia 80 ya walimu walioshiriki katika
utafiti huo uliofanyika katika mikoa sita nchini, walisema Serikali
haijawashirikisha katika uboreshaji wa mtalaa mpya unaotumika sasa, hivyo
wanapata ugumu kuutekeleza.
“Walimu wanabainisha kuwa , hawajashirikishwa katika
mabadiliko ya mtalaa kutoka kwenye maudhui kwenda maarifa yanayomjengea ujuzi
mwanafunzi hali inayosababisha wengi kufundisha kwa mazoea,” alisema na
kuongeza:
“Wengi wa wakuza mitaala na walimu, watekelezaji wa mtaala,
mara chache hushirikishwa katika michakato ya utungaji na kwa ujumla hawaelewi
michakato hii”.
Kuhusu mada kutotungiwa mtihani, Dk Mkumbo alitoa mfano wa
somo la Baiolojia katika mtihani wa 2009, kwamba kati ya maswali 29, matano
(asilimia 1&0 yalitoka kwenye mada moja tu ya usalama katika mazingira).
Somo hilo lina mada 16.
Dk Mkumbo alisema japokuwa Serikali imekuwa ikitekeleza
mtalaa unaomjengea mwanafunzi ujuzi tangu mwaka 2005, ni walimu wachache
wanaoifahamu dhana na falsafa ya mtalaa huo.
Kuhusu alama za mazoezi Dk Mkumbo
alisema hakuna makubaliano kati ya NECTA kwa upande mmoja, walimu na wakuza
mitaala kwa upende mwingine, iwapo mazoezi yanajumuishwa katika mitihani ya
mwisho awa watahiniwa.
Wakati maafisa wa NECTA wakidai kuwa mazoezi hujumuishwa
katika matokeo ya mwisho ya watahiniwa, walimu na wakuza mitaala hawaamini kuwa
kuna utaratibu huu,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti, Habari na Machapisho
wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Makoye Wangeleja alikiri kuwa, taasisi yake
imekuwa ikiwashirikisha walimu kwa kiasi kidogo, hali aliyosema inatokana na
kutokuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kazi hiyo.
“Ni kweli walimu hawajapewa mafunzo kutokana bajeti finyu,
lakini tunapokea mapendekezo ya utafiti huu na kuahidi kuyafanyia kazi, lengo
likiwa ni kuboresha kiwango cha elimu nchini,” alisema Wangeleja.
Akizungumzia ushirikiano wa NECTA na taasisi nyingine
alisema kuwa, mahojiano yaliyofanywa yanaonyesha kuwa mchakato wa
utungaji wa mitihani kwa kiwango kikubwa ni kazi ya maofisa wa NECTA, ijapokuwa
wataalamu wa aina tofauti huombwa ushauri kwa kadri wanavyohitajika.
Mapendekezo,
Pamoja na mambo mengine, Dk Mkumbo alipendekeza kuwa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na wadau wengine elimu waweka utaratibu endelevu wa kuwapatia walimu fursa za mafunzo ya kila mara kuhusu mtalaa mpya.
Pamoja na mambo mengine, Dk Mkumbo alipendekeza kuwa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na wadau wengine elimu waweka utaratibu endelevu wa kuwapatia walimu fursa za mafunzo ya kila mara kuhusu mtalaa mpya.
“Ni jambo muhimu kutafuta namna ya kuwaandaa walimu kujua
dhana, falsafa na mahitaji ya mtalaa unaolenga maarifa ya ujuzi,” aliongeza.
Kadhalika alipendekeza uimarishwe ushirikiano na mawasiliano
kati ya NECTA na Taasisi ya Elimu Tanzania, ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu
mtaala unaomjengea mwanafunzi ujuzi kwa kuzingatia malengo na matokeo ya
kujifunza yanavyopimwa.
Kwa karibu miaka mitano sasa, kiwango cha ufaulu katika
mitihani ya Taifa hasa ya kidato cha nne, kimekuwa kikishuka, kiasi cha kusababisha
mijadala mikubwa ya kitaifa.
Mathalani mwaka 2010 wanafunzi 177,021 sawa na asilimia 50
ya wanafunzi 354,042 waliofanya mtihani wa kidato cha nne walifeli kwa kupata
daraja sifuri. Wanafunzi wengine 136,633, sawa na asilimia 38.6 walipata daraja
la nne.
Utafiti wa HakiElimu ulifanyika katika mikoa sita ya Mwanza,
Tabora, Kilimanjaro, Singida, Morogoro na Iringa ikihusisha walimu na wadau
wengine wakiwamo wakuza mitaala na moafisa wa mitihani.
Na Theophilo
Felix
Chanzo ni gazeti la mwananchi.