Saturday, November 24, 2012


Kasoro katika mchakato utunzi mitihani, mitaala.

UTAFITI wa kitaalamu umeonyesha kuwapo kwa kasoro katika mchakato wa utunzi wa mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na kubainisha kuwa, kufeli kwa wanafunzi wa shule za sekondari kunatokana na walimu kutopewa mafunzo ya utekelezaji wa mitalaa.

Miongoni mwa kasoro zilizobainishwa ni pamoja na utata kuhusu nafasi za alama za mazoezi katika mtihani wa mwisho na ushiriki wa walimu na wakuzaji mitalaa katika utunzi wa mitihani hiyo.

Kadhalika matokeo ya utafiti huo ulioratibiwa na Shirika la HakiElimu, yanaitaja kasoro nyingine kuwa,ni baadhi ya mada za masomo kutungiwa maswali mengi, huku mada nyingine zikiachwa bila kutungiwa maswali kwa muda mrefu.

Hata hivyo, utafiti huo umeweka bayana kuwa, hakuna uhusiano wa moja kwa moja unaothibitisha kuwa mitihani inayotungwa ndio sababu ya wanafunzi kufeli, kwani kwa kiasi kikubwa maswali yanayotungwa yamekuwa yakiakisi kilichomo kwenye mitalaa
.
Akiwasilisha ripoti ya utafiti huo kwa wanahabari na wadau wa elimu jana, Mkuu wa Kitivo cha Elimu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE),  Dk Kitila Mkumbo alisema kuwa, tatizo lililopo ni walimu kutopatiwa mafunzo ya mitalaa, hasa inapofanyiwa uboreshaji na kuwapo kwa mazingira duni ya kufundishia na kujifunzia.

“Kuna ongezeko la wanafunzi kufeli mitihani yao ya mwisho na mara nyingi tumekuwa tukihusisha na sababu nyingine bila kuangalia ushiriki wa walimu katika uboreshaji wa mitaala,” alisema.
Alisema zaidi ya asilimia 80 ya walimu walioshiriki katika utafiti huo uliofanyika katika mikoa sita nchini, walisema Serikali haijawashirikisha katika uboreshaji wa mtalaa mpya unaotumika sasa, hivyo wanapata ugumu kuutekeleza. 

“Walimu wanabainisha kuwa , hawajashirikishwa katika mabadiliko ya mtalaa kutoka kwenye maudhui kwenda maarifa yanayomjengea ujuzi mwanafunzi hali inayosababisha wengi kufundisha kwa  mazoea,” alisema na kuongeza:

“Wengi wa wakuza mitaala na walimu, watekelezaji wa mtaala, mara chache hushirikishwa katika michakato ya utungaji na kwa ujumla hawaelewi michakato hii”.

Kuhusu mada kutotungiwa mtihani, Dk Mkumbo alitoa mfano wa somo la Baiolojia katika mtihani wa 2009, kwamba kati ya maswali 29, matano (asilimia 1&0 yalitoka kwenye mada moja tu ya usalama katika mazingira). Somo hilo lina mada 16.
Dk Mkumbo alisema japokuwa Serikali imekuwa ikitekeleza mtalaa unaomjengea mwanafunzi ujuzi tangu mwaka 2005, ni walimu wachache wanaoifahamu dhana na falsafa ya mtalaa huo.
Kuhusu alama za mazoezi Dk Mkumbo alisema hakuna makubaliano kati ya NECTA kwa upande mmoja, walimu na wakuza mitaala kwa upende mwingine, iwapo mazoezi yanajumuishwa katika mitihani ya mwisho awa watahiniwa.

Wakati maafisa wa NECTA wakidai kuwa mazoezi hujumuishwa katika matokeo ya mwisho ya watahiniwa, walimu na wakuza mitaala hawaamini kuwa kuna utaratibu huu,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti, Habari na Machapisho wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Makoye Wangeleja alikiri kuwa, taasisi yake imekuwa ikiwashirikisha walimu kwa kiasi kidogo, hali aliyosema inatokana na kutokuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kazi hiyo.
“Ni kweli walimu hawajapewa mafunzo kutokana bajeti finyu, lakini tunapokea mapendekezo ya utafiti huu na kuahidi kuyafanyia kazi, lengo likiwa ni kuboresha kiwango cha elimu nchini,” alisema Wangeleja. 

Akizungumzia ushirikiano wa NECTA na taasisi nyingine alisema kuwa,  mahojiano yaliyofanywa yanaonyesha kuwa mchakato wa utungaji wa mitihani kwa kiwango kikubwa ni kazi ya maofisa wa NECTA, ijapokuwa wataalamu wa aina tofauti huombwa ushauri kwa kadri wanavyohitajika.

Mapendekezo,
Pamoja na mambo mengine, Dk Mkumbo alipendekeza kuwa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na wadau wengine elimu waweka utaratibu endelevu wa kuwapatia walimu fursa za mafunzo ya kila mara kuhusu mtalaa mpya.

“Ni jambo muhimu kutafuta namna ya kuwaandaa walimu kujua dhana, falsafa na mahitaji ya mtalaa unaolenga maarifa ya ujuzi,” aliongeza.
Kadhalika alipendekeza uimarishwe ushirikiano na mawasiliano kati ya NECTA na Taasisi ya Elimu Tanzania, ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mtaala unaomjengea mwanafunzi ujuzi kwa kuzingatia malengo na matokeo ya kujifunza yanavyopimwa.
Kwa karibu miaka mitano sasa, kiwango cha ufaulu katika mitihani ya Taifa hasa ya kidato cha nne, kimekuwa kikishuka, kiasi cha kusababisha mijadala mikubwa ya kitaifa.

Mathalani mwaka 2010 wanafunzi 177,021 sawa na asilimia 50 ya wanafunzi 354,042 waliofanya mtihani wa kidato cha nne walifeli kwa kupata daraja sifuri. Wanafunzi wengine 136,633, sawa na asilimia 38.6 walipata daraja la nne.

Utafiti wa HakiElimu ulifanyika katika mikoa sita ya Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Singida, Morogoro na Iringa ikihusisha walimu na wadau wengine wakiwamo wakuza mitaala na moafisa wa mitihani.

Na  Theophilo Felix
Chanzo ni gazeti la  mwananchi.

Friday, November 2, 2012


Mbunge amcharukia waziri Bungeni

  MBUNGE wa Tunduru Kusini, Mtutura Abdallah Mtutura (CCM) jana aliibana Serikali na kuitaka kuacha kutoa majibu ya uwongo ambayo yanapatikana kutoka kwa watuhumiwa.
Mtutura alitoa kauli hiyo baada ya kutokubaliana na majibu ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kuhusu kukanusha kuwa wananchi wa Tunduru hawateswi wala kupigwa wanapoingia kuvua samaki kandokando ya Mto Ruvuma.
“Mheshimiwa Spika, hivi itakuwaje kama nitaleta ushahidi hapa kuwa wananchi wanapigwa, wanateswa na kuporwa mali zao pindi wanapoingia katika maziwa na bahari kwa ajili ya kuvua samaki tu,” alihoji Mtutura na kuongeza.
“Maana ninachoona hapa ni kuwa Naibu Waziri amekuja na majibu ambayo kwa vyovyote ameyapata kutoka kwa watuhumiwa wa jambo hilo ndio maana anajibu hivyo majibu ambayo sikubaliani nayo.”
Katika swali la msingi Mbunge huyo alitaka kujua kwa nini wananchi wa Vijiji vya Wenje, Nasomba Makande, Kazamoyo, Misechele na Meyamtwaro vilivyo kandokando ya Mto Ruvuma wanasumbuliwa na askari wa maliasili kwa kupigwa na kunyang’anywa mali zao wanapovua samaki kama kitoweo.
Naibu Waziri alisema kuwa kutokana na wananchi wengi kuharibu mazingira kwenye maeneo ya wazi, kumesabisha upatikanaji mdogo wa samaki na hivyo hulazimika kuingia kwenye pori la Mwambesi kinyume na sheria na kuvua samaki huko.
Alisema wananchi hao wanapokutwa katika maeneo hayo, hukamatwa na kikosi cha doria na kupelekwa katika kituo cha Polisi kama taratibu za nchi zinavyoelekeza.
Hata hivyo alibainisha kuwa yapo matukio kadhaa ambayo hubainika kwa kisingizio cha kuvua samaki, lakini wananchi wanaingia na kufanya ujangili ndani ya hifadhi.
Waziri alilieleza kuwa Bunge kuwa hali ya ujangili hivi sasa ni kubwa nchini na majangili wengi huingia ndani ya hifadhi kwa lengo baya huku wakiwa na silaha nzito zikiwamo za kivita hivyo ni vema hata askari wa wanyamapori kuwa makini na jambo hilo.

Imewekwa na Moi Dodo
Chanzo ni gazeti la Mwananchi