Monday, January 16, 2012


   Pacha wa marehemu Regia mtema bi. Remjia mtema akiwa na gang gongo alilokuwa akilitumia marehemu pacha wake



PACHA wa Mbunge wa Viti Maalum Chadema, Regia Mtema (32) aliyefariki juzi kwa ajali ya gari eneo la Ruvu mkoani Pwani, Remija Mtema (32) ameeleza alivyonusurika baada ya kushuka kwenye gari muda mfupi kabla ya ajali.

Akizungumza naTumaini habari  jana, Remija ambaye ni kurwa, alisema Regia kabla ya ajali iliyosababisha kifo chake, alikuwa akitoa kauli za kutia moyo na za kutarajia kuonana tena.

“Tulitoka nyumbani kwake Mbezi-Makabe, Dar es Salaam kwenye saa tatu asubuhi, mimi nilikuwa nakwenda Iringa na tuliondoka na gari lake hilo lililopata ajali nyumbani hapo, wakanishusha Mbezi stendi nisubiri basi la Iringa .

“Wakati tunatoka nyumbani alikuwa anaongea kwa uchangamfu sana, kwanza juzi (Ijumaa)
tulizungumza na kupanga kwamba mimi niende Iringa kuomba ruhusa kazini, maana kuna wakati nikiwa huru namsaidia kazi kama Katibu wake, tulipanga nikipewa ruhusa nirudi nimsaidie kwenye Kamati na Bungeni,” alisema Remija.

Kwa mujibu wa Remija, walikubaliana hivyo na baada ya kupanga mambo yao usiku huo wa
Ijumaa, walicheza sana karata.

“Ni karata za kuagana maana mimi ndio nilikuwa nasafiri kesho yake kwenda Iringa, asubuhi ndio tukaondoka huku tunacheka, mimi nikashukia Mbezi, alikuwa ni zaidi ya pacha wangu, alikuwa rafiki yangu,” alisema Remija.

Remija ambaye ni Ofisa Tarafa wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, alisema aliposhuka Mbezi
kusubiri gari, walikaa nae na watu wengine kwenye gari kwa karibu saa moja wakimsubiri mama yao, Bernadeta aliyekuwa akitokea Tabata-Chang’ombe nyumbani kwao.

“Mama alipofika aliingia garini na wakaondoka, pacha akasisitiza nikipata usafiri niwaambie, ni
kama alitamani niendelee nao lakini haikuwa hivyo, baada ya muda wa nusu saa mama alipiga simu kuniuliza kama nimepata basi maana waliona basi la Upendo limewapita, nikamjibu bado, baada ya muda mfupi nikapata basi la Budget,”

“Nilipoingia kwenye basi saa tano asubuhi hivi, nikamtumia ujumbe Regia kuwa nimepata basi, lakini ujumbe haukujibiwa, nikajua labda kwa kuwa alikuwa anaendesha gari, nikaendelea kusoma gazeti na tulipofika Ruvu niliona watu lakini sikutilia maanani nikaendelea kusoma gazeti,” alisema Remija.

Alisema kabla hajafika Chalinze, alipigiwa simu na mama yake kuwa wamepata ajali na
wapo Hospitali ya Tumbi na kumuomba dereva ashuke kwa kuwa ndugu zake wamepata ajali
Ruvu.

“Dereva na kondakta waliniuliza aina ya gari, nikawaambia wakathibitisha waliiona. akasimamisha gari nikashuka na kuanza safari ya kurudi hadi Hospitali ya Tumbi, nikakuta kweli Regia amefariki,” alisema Remija.

Alisema pacha wake alikuwa jasiri ambaye akiamua jambo lake ni lazima alifanye, alikuwa na huruma asiyependa mtu aonewe na alimuamini Mungu kwa kila jambo kutokana na malezi ya kiimani waliyopata kwa baba na mama yao mlezi.

Kwa mujibu wa Remija, yeye na pacha mwenzake walizaliwa Hospitali ya Ocean Road, jijini Dar
es Salaam Aprili 21 mwaka 1980, alikuwa mpenzi na shabiki wa timu ya mpira wa miguu ya Simba kwa hapa nchini na kwa nje alikuwa akipenda kufuatilia Barcelona ilipocheza zaidi ya timu nyingine.

Baba wa marehemu, Estelatus Mtema aliliambia gazeti hili jana kuwa anamshukuru Mungu kwa
kila jambo na kuomba majeruhi akiwemo mkewe waliolazwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili walikohamishiwa wakitokea Tumbi juzi jioni, wapone mapema.

Utaratibu wa maziko

Mtema alisema misa itafanyika leo saa tisa alasiri katika Kanisa Katoliki la Segerea pamoja na heshima za mwisho na kesho kutakuwa na heshima za mwisho katika ukumbi wa Karimjee.

Alisema bada ya hapo safari ya kulekea Ifarakara itaanza na maziko yatakuwa Jumatano huko
Ifarakara mjini nyumbani kwa wazazi wa marehemu.

Majeruhi Muhimbili
Mtoto wa binamu wa mama wa marehemu, Theresia Simon, ambaye ilidaiwa kuwa amefariki
kutokana na kujeruhiwa vibaya kichwani, anaendelea vizuri alikolazwa wodi namba 10 Kibasila.

Theresia katika mahojiano, alisema anamshukuru Mungu hali yake inaendelea vizuri na maumivu yamepungua.

Baadhi ya vyombo vya habari jana, viliripoti kuwa Theresia aliyejeruhiwa kichwani, alikufa hivyo kufanya idadi ya walioaga dunia kuwa wawili akiwemo Mbunge Mtema.

Shangazi yake, Consolata Mwandenga alisema pia kuwa alimpa uji jana na kula vizuri asubuhi na mchana hivyo hali yake ni njema. Pia mama wa marehemu, Bernadeta na watu wengine
wawili, wanaendelea vizuri na wote wamelazwa katika wodi hiyo.

Vikao vya dharura Chadema
Wakati huo huo Sekretarieti ya Chadema jana ilifanya kikao cha dharura chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa kupanga utaratibu wa chama na viongozi wake wakuu, kushiriki kikamilifu kwenye maombolezo, heshima za mwisho na hatimaye maziko yaliyopangwa kufanyika Ifakara.

Shughuli hizo za mazishi ya heshima kwa Mbunge huyo, kwa mujibu wa taarifa za Chadema, zitaongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe.

Mbali na Sekretarieti, pia Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa Chadema, ilifanya kikao cha
dharura, kwa kuzingatia uzito wa msiba uliotokea na kupitisha azimio kwamba wabunge wote wa Chadema washiriki kutoa heshima ya mwisho.

Kwa mujibu wa azimio hilo, wabunge wote wa chama hicho watasindikiza mwili wa Regia
hadi Ifakara na kushiriki maziko.
                                                                                                            Na SOLOMON LEKUI

Sunday, January 15, 2012

Chadema yagubikwa na simanzi:yapoteza mbunge

                                        Mbunge Regia Mtema; enzi za uhai wake 


Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Regia Estelatus  Mtema (32), amefariki dunia baada ya gari alilokuwa akiendesha, kupinduka eneo la Mlandizi, Kibaha mkoani Pwani jana.

Ajali hiyo ilitokea saa 5:30 asubuhi karibu na Sekondari ya Ruvu, wakati mbunge huyo na watu wengine saba, wakisafiri kwa gari aina ya Toyota Landcruiser wakitoka Dar es Salaam kwenda Morogoro.Akielezea mazingira ya ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu, alisema mbunge huyo alifariki baada ya gari hilo alilokuwa akiendesha mwenyewe, kuacha njia na kupinduka.

Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya Mtema kujaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake na ghafla aliona gari lingine likija kasi mbele yake,  katika kujaribu kulikwepa, ndipo gari hilo lilipinduka.

"Wakati akiwa hajalipita gari hilo aliliona gari lingine likija mbele kwa kasi , katika kulikwepa wasigongane uso kwa uso, alitoa gari lake barabarani na kusababisha kupinduka,’’ alisema Mangu.

Alisema watu wengine saba  waliokuwa kwenye gari hilo walijeruhiwa, wawili kati yao  hali zao zilikuwa mbaya,  walipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, huku wengine watano, wakiwahishwa Hospitali Teule ya Tumbi Kibaha.

                                    Gari iliyopelekea kifo cha mbunge ikiwa 
                                   imepakiwa kituo cha polisi Mlandizi mkoani pwani.

Aliwataja majeruhi waliolazwa Tumbi kuwa ni Lawrence Mtokambali (58), Benadetha Mtema (50), Peter Madesa (50) na Rogers Abdallah(18).

Chadema yatoa tamko
Chadema kilisema kuwa Mtema alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho na Waziri Kivuli wa Kazi na  alikuwa mchapa kazi hodari katika majukumu mbalimbali yakiwepo ya kijamii na kisiasa.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Chadema jana na kusainiwa na Katibu Mwenezi wa chama hicho, John Mnyika ilieleza kuwa viongozi wakuu wa chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Willibroad Slaa, wajumbe wa Kamati Kuu, Wakurugenzi wa chama hicho makao makuu na wabunge, wameshtushwa na kifo hicho na kuungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Chadema kimesema taarifa zaidi kuhusu taratibu za maziko, itatolewa mara baada ya kukamilisha majadiliano kati familia ya marehemu, chama na Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kufuatia kifo hicho, mkutano wa Chadema uliokuwa umepangwa kufanyika jana Mjini Kibaha umehirishwa hadi itakapotangazwa wakati mwingine.

Elimu yake
Mtema alizaliwa Aprili 21, 1980. Alisoma elimu ya msingi kati ya mwaka 1989 na 1995. Alijiunga na Shule ya Sekondari Forodhani, Dar es Salaam mwaka 1996 hadi  1999 na kuhitimu kidato cha nne.
Aliendelea kidato cha tano 2002 na sita kati ya mwaka 2000 na 2002 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Machame, mkoani Kilimanjaro.

Mwaka 2003 hadi 2006 alisoma Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na kupata Shahada ya Maarifa ya nyumbani na Lishe. Baada ya kuhitimu shahada yake, marehemu Mtema alifanya kazi katika taasisi mbalimbali kabla ya kujiunga na Chadema na kuteuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana ya chama hicho.

Baadaye aliteuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Mafunzo ya chama hicho, nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka 2010 alipoteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum.

JK amtumia rambirambi Mbowe
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kufuatia kifo cha mbunge huyo.

Katika salamu hizo, Rais ameelezea kusikitishwa kwake na taarifa za kifo cha mbunge huyo na kueleza kwamba, marehemu Mtema  amepoteza maisha akiwa kijana na kwamba pigo hilo si kwa Chadema pekee bali kwa taifa zima.

“Nimepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi habari za kifo cha Mheshimiwa Mtema katika ajali ya gari. Siyo kwamba ajali hii imechukua maisha ya kijana bali imelinyang’anya taifa mbunge hodari, na kwa hakika, kifo chake siyo tu ni pigo kwa chama chako bali ni pigo kwa sote na kwa taifa letu kwa jumla.

"Nakutumia wewe binafsi, chama chako na wanachama wake salamu za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo na msiba huu mkubwa," alisema Rais Kikwete kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.

Aliongeza: “Napenda ujue kuwa niko nanyi katika msiba huu. Napenda vilevile uniwasilishie salamu zangu za rambirambi za dhati kabisa kwa wana-familia, ndugu na jamaa wa marehemu Mheshimiwa Mtema.

Taarifa hiyo imemwomba Mbowe kufikisha salamu za Rais Kikwete kwa familia ya mbunge huyo na kuijulisha kuwa amepokea habari hizo kwa huzuni kubwa. "Wajulishe kuwa nawaombea kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, awajalie uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi yake.

Wananchi wamlilia
Katika kuonyesha kuguswa na kifo hicho mamia ya watu wanaotumia mtandao wa kijamii maarufu kwa jina la ‘Facebook’  walielezea kusikitishwa na kifo hicho huku wakitoa maoni mbalimbali.

Miongoni mwa maelezo yao ni juu ya maneno aliyowahi kuyazungumza mbunge huyo kijana, ukiwamo ujumbe alioandika katika mtandao huo akiwataka wananchi wamweleze kero zao ili azifikishe katika mkutano ujao wa Bunge.

Ujumbe huo aliouandika Januari 10 mwaka huu na kuungwa mkono na watu 159 ulisomeka hivi;

“Wapenzi, habari zenu kama una kero yoyote unayoona inafaa ikasemewe bungeni au nje ya Bunge na Wabunge na Viongozi wa Chadema basi tupia hapa kero yako. Angalizo; isiwe kero binafsi..., karibuni sana pamoja tunaweza”.

Mtema anakuwa mbunge wa pili wa chama hicho kufariki dunia kwa ajali ya gari, Julai 27, 2008 Mbunge mwingine wa chama hicho Jimbo la  Tarime, Chacha Wangwe alikufa katika ajali ya gari eneo la Pandambili mkoani Dodoma.
                                                                                                                     posted by Frank Kimaro
                                 

Thursday, January 12, 2012

Salam kutoka Finland

Waziri wa Habari na Mahusiano ya Umma, TUSO IUCO, Elisha Magolanga akiwa nchini Finland kuhudhuria mafunzo (Exchange programme) katika chuo cha Turku University Applied of Sciences
Katikati ya jiji la Turku, mji

Katika sherehe ya kuwakaribisha wanafunzi wote waliohudhuria exchange programme katika Hotel ya Holiday Inn mjini Turku