ABEL LOSHILAA MOTIKA,MR.EBBO. Enzi ya uhai wake.
Na John Alex.
Wakazi wa mkoa wa Iringa na vitongoji vyake,wameeleza hisia zao kwa masikitiko kufuatiwa kifo cha msanii wa nyimbo za bongo fleva,mtayarishaji na mmiliki wa studio ya Motika record iliyoko mkoaniTanga Abel Motika almaarufu kama Mr.Ebbo.
Wakizungumza na Tumaini habari kwa nyakati na amzingira tofauti wananchi hao hususan vijana wameelezea kushtushwa kwao na kifo cha msanii huyo nguli wa bongo fleva ambaye amekuwa akiimba kwa kwa kutumia lafudhi ya kabila lake la Wamasai.
Aidha wameeleza kuwa kifo cha Mr.Ebbo ni pigo kubwa sana katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini na hata nje ya nchi kwani kazi zake nzuri zimewezesha utamaduni wa Taifa la Tazania kutangazwa kimataifa kutokana na staili aliyokuwa akiitumia ya kabila lake ambalo ni wenyeji wa Tanzania.
Kutokana na ujumbe uliokuwa ndani ya nyimbo zake hasa katika kuhamasisha maendeleo na kudumisha amani na umoja msanii huyu nguli amejizolea umaarufu mkubwa sana nchini jambo lililomfanya apendwe na watazania wote bila kujali kabila dini wala rangi.
“Sisi wakazi wa Iringa tumepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa za kifo cha msanii huyu maarufu kipenzi cha watanzania na kwa kweli kifo chake ni pigo kubwa sana kwa taifa letu kwani alikuwa ni mhamasishaji mzuri sana wa maendeleo katika taifa letu na aliuwakilisha vizuri sana utamaduni wa mtanzania kimataifa na kiukweli ataendelea kukumbukwa daima kwa mchango wake katika kuutangaza utamaduni wa mtanzania”anamalizia kusema Rahim Mdemu mkazi wa Kihesa manispaa ya Iringa.
Kwa upande wake Abeid Maila mwanafunzi wa Tumaini Iringa ameeleza kuwa Mr.Ebbo ataendelea kukumbukwa daima kwa bururdani yake nzuri aliyokuwa akiitoa na hasa kwa mtindo wa uimbaji wake kwa lafudhi ya kabila lake ,na pia ni pigo kwa tasnia nzima ya muziki wa kizazi kipya hapa nchini.
“Kwa mara ya kwanza nimemfahamu Mr.Ebbo hasa alivyotamba na nyimbo yake ya kwanza ya “Mi mmasai bana”ambayo kimsingi ndiyo iliyomtoa hata hivyo nyimbozake wengi wanachukulia tu kuwa zinachekesha tu lakini hata kuelimisha.Kimsingi pengo aliloacha halitaweza kuzibika kamwe kwani hakuna atakayeweza kuiga staili ya uimbaji wake”
Kwa upande wa wanamuziki mkoani Iringa,Tumaini habari ilibahatika kukutana na Kijana mwanamuziki na msanii wa nyimbo za Hip hop mkoani Iringa anayefahamika kwa jina la Honorius Haule almaarufu kama Honorius. “Nitamkumbuka daima Mr.Ebbo kwa mchango wake mkubwa katika kukuza,kutangaza na kudumisha utamaduni wa mtanzania”alimalizia Honorius.
Mr.Ebbo amefariki mwishoni mwa wiki iliyopita katika hospitali ya misheni ya USA river iliyoko mkoani Arusha alikokuwa amelazwa kwa muda kidogo.
No comments:
Post a Comment