Saturday, December 31, 2011

Mwaka uliokua na upinzani mkubwa katika medani ya siasa kati ya CHADEMA na C.C.M

By Frank Kimaro













MWAKA 2011 unamalizika leo na kuacha kumbukumbu ambazo ni vigumu kusahaulika katika medani za siasa nchini, huku baadhi ya vigogo wa kisiasa wakiweka historia kutokana na kukumbwa na matukio ya aina yake.
Katika miezi 12 iliyopita, Taifa limepita katika misukosuko mingi ya kisiasa iliyoanzia Januari 5, pale maadamano ya Chadema yaliyofanyika mjini Arusha yaliposababisha vifo vya watu wanne.

Hilo ni miongoni mwa matukio mengi ya kisiasa ambayo yalikuwa na sura ya mvutano baina ya vyama vya CCM na Chadema, ambavyo hivi sasa vinatoa mwelekeo wa siasa za nchi.

Risasi za moto na mabomu ya machozi vilitumika katika jitihada za polisi kuzima maandamano hayo, wakitekeleza amri ya Mkuu wa Jeshi hilo, Inspekta Jenerali Saidi Mwema ambaye awali alipiga marufuku maandamano hayo kwa madai ya kuwepo uwezekano wa kutokea vurugu.

Kufuatia vurugu hizo, Januari 6 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa, wabunge wawili wa chama hicho na wafuasi wengine 21, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kujibu mashitaka kuhusu maandamano hayo, kesi ambayo bado inaendelea hadi sasa.

Kiini cha mtafaruku huo ni mvutano kuhusu nafasi ya Meya wa Jiji la Arusha, ambayo Chadema walikuwa wakilalamikia kwamba uchaguzi ulichakachuliwa hivyo kukipa CCM ushindi hivyo kufanya maandamano ya kupinga uchaguzi huo.

Hadi leo suala hilo limebaki kuwa kitendawili kisichokuwa na majibu kwani kumekuwapo kwa migogoro ya chinichini kuhusu suala zima la meya kiasi cha kuathiri shughuli za maendeleo katika mji huo wa kitalii na kibiashara uliopo Kaskazini Mashariki mwa Tanzania.

CCM na Chadema viliendeleza siasa za kupimana ubavu katika uchaguzi mdogo wa Igunga ulitokana na kujiuzulu kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia CCM, Rostam Aziz, ikiwa ni hatua ya kutekeleza falsafa ya ‘kujivua gamba’ iliyoasisiwa na chama chake ikiwataka watuhumiwa wote wa ufisadi ndani ya chama hicho kuachia ngazi.

Uchaguzi mdogo wa Igunga ulikuwa uwanja mwingine wa mapambano baina ya Chadema na CCM, kwani kuliendeshwa siasa chafu ambazo zilizosababisha baadhi ya watu kujeruhiwa na kufanyiwa vietendo vya kinyama.

Hata hivyo CCM walifanikiwa kutetea jimbo hilo kupitia kwa mgombea wake, Dk Dalaly Kafumu aliyemshinda kwa kura zaidi ya 3,000 mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huo, Joseph Kashindye wa Chadema.

Ndani ya Chadema
Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willbrod Slaa ambaye alikuwa mgombea urais kupitia chama hicho mwaka jana, amekuwa kimya kwa muda mrefu na ni mara chache kuonekana hadharani akizungumza, isipokuwa katika matukio ya chama chake.

Hali hiyo inatafsiriwa kwamba huenda bado akawa na mpango wa kugombea nafasi hiyo mwaka 2015 akimsubiri mteule wa CCM ambaye licha ya harakati ndani ya chama hicho bado hajafahamika.

Mwenyekiti wake Freeman Mbowe anapewa sifa ya kuweza kuwamudu nakuwavumilia makada wa chama hicho wengi wakiwa vijana wenye mihemko ya kisiasa na kutaka hatua za haraka katika mambo mengi.

Wachunguzi wa siasa ndani ya Chadema, wanasema uwezo wa Mbowe akiwa Mwenyekiti na Kiongozi wa Upinzani Bungeni ameweza kuwamudu wabunge vijana ambao ni machachari wakiwamo, Halima Mdee (Kawe), Ezekia Wenje (Nyamagana), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), Godbless Lema (Arusha Mjini) na wengineo.
Jaribu kubwa la Mbowe lilikuwa ni kauli za Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda ambaye mara kadhaa alitoa matamshi kinyume cha msimamo wa Chadema lakini Mbowe hakuwahi kukubali Chadema kupoteza muda katika suala hilo.

Hata hivyo changamoto katika chama hicho kikuu cha upinzani nchini ni jinsi kitakavyosimamia uchaguzi wake wa ndani mwaka 2014 na uteuzi wa mgombea wa urais na wabunge mwaka 2015.

Ndani ya CCM
Mwaka huu, ndani ya CCM jina la Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa lilitikisa vyombo vya habari hasa pale alipoamua kuvunja ukimya na kuweka bayana kile alichodai kuwa ni ukweli kuhusu sakata la Richmond ambalo limekuwa likimwandama tangu alipolazimika kuachia madaraka Februari 2008.

Lowassa katika NEC ya CCM iliyopita, aliweka wazi kwamba kumwandama kwa suala la Richmond ni kumwonea kwani hata Rais Jakaya Kikwete anafahamu kilichojiri.

Hata hivyo, wafuatiliaji wa siasa za ndani ya CCM wanaiona hatua hiyo ya Lowassa kwamba inamweka katika hatari kubwa ya kubanwa zaidi hasa kutokana na kumtaja Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kwamba alikuwa akijua kila kilichoendelea kuhusu Richmond.

Lowassa ni mmoja wa watu waliokuwa wakitajwa kwamba wanatakiwa kujivua gamba, mpango ulioasisiwa na Rais Kikwete kuwataka watuhumiwa wa kashfa mbalimbali hasa za ufisadi ndani ya chama hicho tawala, kuachia kwa hiari yao nafasi za uongozi walizonazo.

Tangu azimio la kuwataka watuhumiwa hao kujiuzulu kwa hiari yao litolewe ilipita miezi saba ambayo ilishuhudia historia ikiandikwa katika media ya siasa nchini, kufuatia kujiuzulu kwa Rostam.

Kujiuzulu kwa Rostam ambaye anatajwa kuwa mshirika wa karibu wa Rais Kikwete kwa upande mmoja na Lowassa kwa upande mwingine, ilitafsiriwa kuwa inadhoofisha moja ya makundi ambayo yamo ndani ya CCM.

Hata hivyo Rostam alijiuzulu huku akilalama kuhusu kile alichokiita siasa uchwara zinazoendeshwa ndani ya CCM na kuwataja, Nape Nnauye ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara), John Chiligati kuwa chanzo cha siasa hizo.

Wanasiasa vijana
Nape ni mmoja wa wanasiasa vijana waliog’ara katika siasa za Tanzania 2011 hasa pale alipoteuliwa kuwa mmoja wa wajumbe wa Sekretarieti mpya ya CCM inayoongozwa na Katibu Mkuu, Willson Mukama.

Kung’ara kwa Nape kunatokana na kile kinachotajwa na wachunguzi wa siasa za hapa nchini kwamba ni ujasiri wa kusema bila woga kile anachokiamini, pasipo kujali wabaya wake ambao wamekuwa wakikwandama kwamba anasababisha mgawanyiko ndani ya chama chake.

Ujasiri wake huo ndio uliababisha kupangwa njama za kumvua wadhifa wake katika vikao vya juu vya CCM vilivyofanyika mwishoni mwa Novemba mwaka huu mjini Dodoma, mpango ambao hata hivyo haukupata hata nafasi ya kujadiliwa hasa pale suala la kujivua gamba liliporejeshwa Kamati Kuu kwa maana ya kuwashughulikia kinidhamu wale wote wenye makosa ambao hawakufuata nyayo za Rostam kujiuzulu nyadhifa zao.

Ndani ya vyama vya upinzani, David Kafulika ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kusini kupitia NCCR Mageuzi alijikuta akitimuliwa uanachama pale alipoonekana kuwa tishio kwa mwenyekiti wake, James Mbatia.

Kafulila ambaye hata hivyo amri ya kufukuzwa kwake imesitishwa na Mahakama Kuu alikofungua kesi kupinga kufukuzwa huko, ni mwanasiasa ambaye amekuwa mahiri katika ujenzi wa hoja hasa ndani ya Bunge ambako aliwahi kuibua sokomoko pale alipowataja kwa majina wabunge watatu wa  CCM  kwa tuhuma za kupokea rushwa wakiwa kazini.

Suala hilo hadi leo limebaki kuwa kiporo kisichoguswa kwani Spika wa Bunge, Anne Makinda hajawahi kuthubutu  kutoa mwongozo ulioombwa na wabunge wawili kuhusu tuhuma hizo akiwamo Godfrey Zambi wa Mbozi Magharibi (CCM) ambaye ni mmoja mwa waliotajwa.

Mwanasiasa mwingine kijana ni January Makamba, mtoto wa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuph Makamba. January kama ilivyo kwa Nape ni mmoja wa wajumbe wa sekretarieti ya CCM inayoongozwa na Mukama.

Kadhalika Mbunge huyo wa Bumbuli ameiongoza Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambako yeye ni Mwenyekiti, kuibana Serikali hasa katika masuala ya umeme kiasi cha kutuhumiwa kwamba ana malengo binafsi ya kutaka kuwa Waziri wa Nishati na Madini, inayoongozwa na Waziri mwingine kijana, William Ngeleja.

Mbali na kuihenyesha Serikali katika masuala ya Umeme, kamati yake katika bunge lililopita iliibua uozo katika sekta ya gesi, pale ilipoweka bayana kwamba Kampuni ya Pan African Energy imekuwa ikiibia Serikali Tanzania mamilioni ya fedha.

Zitto Kabwe ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ameendelea kuwa kipenzi cha Watanzania wengi hasa vijana licha ya ujio wa vijana wapya hasa katika Bunge ambako aliibukia mwaka 2005.

Zitto katika siku za karibuni ameonyesha umahiri mkubwa katika masuala ya fedha na uchumi, amekuwa akivutana na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo kuhusu hali ya uchumi na nchi.

Wakati wa Bunge la Bajeti alivutana na Mkulo kiasi cha kuweka nadhiri kwamba ikibainika kwamba amekula rushwa angejiuzulu Ubunge, huku akimtaka Mkulo naye kuweka nadhiri hiyo. Mkulo hakukubali.

Tundu Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki akiwa mgeni katika siasa za Bunge, amekuwa mwiba mkali katika masuala ya utunzi wa sheria na mara kadhaa amekuwa akiwahenyesha wabunge wa CCM na Serikali bungeni.

Hotuba yake ya mwisho bungeni ni kuhusu muswada wa sheria ya marekebisho ya Katiba, ambayo ilifanya uchambuzi wa nafasi ya Tanzania Zanzibar katika muungano kiasi cha kuwakasirisha sana wabunge wa Visiwani humo.

Chadema waliamua kutoka nje kutokubaliana na kuendelea kujadiliwa kwa muswada huo ambao walisema kuingizwa kwake bungeni na kusomwa kwa mara ya pili, kulikuwa ni batili kwani ulitakiwa usomwe kwa mara ya kwanza kutokana na mabadiliko mengi ikiwa ni pamoja na kuandikwa kwa Kiswahili.

Ndani ya CUF
CUF wanahitimisha mwaka 2011 wakiwa katika mgogoro mkubwa wa kiongozi kufuatia vita baina ya Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed ambaye anataka kuwania nafasi ya Seif.

Mgogoro huo unaendelea kukiweka chama hicho katika wakati mgumu hasa ikizingatiwa kwamba kuingia kwake katika maridhiano na CCM na kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa Tanzania Visiwani kulikiathiri kwa kiasi kikubwa.

Katika baadhi ya uamuzi wake hasa ndani ya Bunge, CUF kimekuwa kikionekana kuegemea upande wa Serikali na mara kadhaa kumekuwa na tuhuma kwamba ni CCM ‘B’.

Katika uchaguzi wa Igunga mgombea wake Leopold Mahona alipata kura zaidi ya 2,000 zikiwa ni pungufu kwa kura 7,000 ikilinganishwa na idadi ya kura ambazo mgombea huyo huyo alipata katika uchaguzi wa 2010.


Hizo ni baadhi ya takwimu zinazoonesha wazi jinsi ambavyo mwaka 2011 ulivyokua na upinzani na mikwarunzano ya hapa na pale hususani katika medani nzima ya siasa hapa nchini, Katika hayo viongozi wanapaswa kujifunza na kuepuka mikwaruzano inayoweza kuleta maafa kwa jamii hususani katika mwaka huu mpya wa 2012.                                                                                       

No comments:

Post a Comment