Thursday, June 28, 2012

MADAKTARI WAPATAO 72 WASIMAMISHWA KAZI MKOANI MBEYA.

  
Na  Consolata Haule

                
            Bodi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, imewafukuza madaktari wapatao 72 kwa   kosa la kutoingia kazini kwa siku tano jambo ambalo ni kinyume cha makubaliano ya mkataba wao wa kazini.
  
          Inasemekana  kuwa madaktari hao ambao 54 ni wale wa mafunzo ambao waliingia mkataba wa miaka miwili na hospitali ya Rufaa na madaktari 18 ni wale walioajiriwa na Wizara ya afya. 
          
         Mwenyekiti wa Bodi Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Norman Sigara, alisema kitendo cha madaktari kutoripoti kazini kwa siku tano ni ukiukwaji wa kanuni za utumisha wa umma hivyo kupitia kanuni hiyo ya utumishi wa umma madaktari hao wamesimamishwa kazi na kurudishwa kwa mwajiri wao ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa hatua zaidi za kinidhamu alizidi kunena.
        
        Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Bodi, imeelezwa kuwa siku ya tarehe 23/6/2012 wafanyakazi 15 waliokuwa zamu hawakufika kazini na tarehe 24/6/2012 wafanyakazi 19 hawakufika kazini. 
        
       Alizidi kusema kuwa kuanzia tarehe 25/6/2012 hadi leo imethibitika kuwa 72 hawakufika kazini hadi leo tarehe 28/6/2012.Na mnamo tarehe 25/6/2012 bodi ya hospitali ilifanya kikao cha dharura ili kujadili hali ya utendaji kazi na utoaji huduma hospitalini na kutoa uamuzi juu ya jambo ilo.
        
       Aliyataja maamuzi hayo kuwa ni Mwenyekiti wa Bodi akutane na madaktari ambao hawakufika kazini ili awasikilize sababu za kutofika na kujadili namna ya kumaliza matatizo hayo jambo ambalo madaktari hao waligoma.

      Baada ya madaktari hao kukaidi ombi hilo, Bodi ya hospitali iliwaandikia barua za kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuvunja mkataba walioingia na hospitali na pia kukiuka kanuni za kudumu za utumishi wa umma nalo walilikaidi
      Alizidi kuongeza kwamba iwapo madaktari ambao hawakuripoti au kueleza sababu za kuridhisha ifikapo mpaka  tarehe 28/6/2012na kwa kuzingatia kanuni za utumishi wa Umma, madaktari hao watasimamishwa kazi na kurudishwa kwa mwajiri wao ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
      
      Vilevile  alisema kuwa kwa ujumla madaktari hao waligomea barua zote mbili yaani ya kuitwa kwenye kikao pamoja na ile ya kuwataka kujieleza hivyo Bodi imechukua hatua za kisheria za kuwafukuza kazi.
    
      Hata hivyo Mwenyekiti huyo wa bodi, alisema kuwa tayari hospitali ya Rufaa kwa ushirikiano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, madaktari watano wamepatikana ili kusaidia huduma kwa hospitali hiyo.





             
                       Mwenyekiti wa Bodi Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Norman Sigara akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu kufukuzwa kazi kwa madaktari hao wapatao 72.

No comments:

Post a Comment