Waraka no. 1 wa mwaka 2012 wa Mbunge kwa Wananchi- “Ukweli ni Uhuru”- Mnyika.
Na Moi Dodo.
Waheshimiwa Wananchi wenzangu,
Amani iwe kwenu,
Kwa kipindi cha wiki nzima kumekuwepo na mjadala mkali bungeni, kwenye
vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na katika taifa kwa ujumla juu ya
bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/13 sanjari na yaliyojiri
kutokana na kauli niliyotoa bungeni juu ya udhaifu wa Rais katika
usimamizi wa maandalizi na utekelezaji wa bajeti pamoja na mipango
muhimu ya maendeleo. Ukweli ni uhuru!.
Aidha, kupitishwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa Fedha
2012/2013 na Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha
2012/2013 bila marekebisho yoyote ya msingi pamoja na michango mingi ya
wabunge ya kukosoa kumedhihirisha kile nilicho tahadharisha tangu awali
kwamba; kwa kuwa udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu kubwa kwa Rais juu ya
bajeti na uendeshaji wa nchi, udhaifu wa Rais una athiri maisha ya
wananchi. Ukweli ni Uhuru!.
Katika mazingira haya, udhaifu wa rais na uzembe wa bunge unapandikiza
migogoro kati ya wananchi na serikali kutokana ufisadi na masuala ya
maendeleo kutopewa kipaumbele cha kutosha zaidi ya matumizi ya kawaida
lakini pia inachochea pia migomo baridi ya watumishi wa umma hususun
madaktari, walimu na askari kutokana pia na madai yao ya muda mrefu
kutokuzingatiwa kwenye bajeti. Ukweli ni Uhuru!.
Kadhalika udhaifu wa kanuni za Kudumu za Bunge umefanya wabunge kuwekewa
mipaka kwa mujibu wa kanuni 97 (2) ya kuchangia mjadala kuhusu hotuba
ya bajeti kwa kuchangia tu mambo ya ujumla yanayohusiana na hali ya
uchumi wa nchi na kwamba mbunge yoyote haruhusiwi kupendekeza mabadiliko
katika makadirio ya mapato na matumizi ya serikali. Ukweli ni Uhuru!.
Pia, katiba imempa mamlaka makubwa Rais juu ya Bunge kwa kuwa Bunge
likikataa bajeti ya serikali kwa mujibu wa Ibara ya 90 (2) (b) moja kwa
moja Rais analivunja bunge suala ambalo huwapa hofu wabunge wengi
hususani wa chama kinachotawala na kuwafanya wapige kura ya NDIO hata
kama waliikosoa bajeti husika. Hivyo, udhaifu wa bunge unachangiwa na
ukweli kwamba katiba imeweka nguvu kubwa kwa Rais katika kuvunja bunge
linapokataa bajeti wakati huo huo kanuni zimekataza wabunge kupendekeza
mabadiliko katika bajeti; kwa hivyo wabunge hawana uwezo wa kubadilisha
na wakati huo huo wakikataa bunge linavunjwa, katika mazingira haya
udhaifu wa Rais wa kushindwa kutumia nguvu hizo za kikatiba una madhara
makubwa sana kwa nchi na maisha ya wananchi. Ukweli ni Uhuru!.
Kwa mantiki hiyo, katika mchakato wa katiba mpya ni muhimu kwa wananchi
kutoa maoni ya kuwezesha ukuu na uhuru wa bunge katika kuisimamia
serikali kwenye mchakato wa bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo na
kuboresha maisha ya wananchi. Wakati katiba mpya ikisubiriwa, ni muhimu
kwa marekebisho ya haraka kufanyika katika kanuni za kudumu za bunge
hususani sehemu ya tisa inayohusu utaratibu wa kutunga sheria kuhusu
mambo ya fedha kuanzia kanuni ya 94 mpaka kanuni ya 107 ili kuongeza
nguvu za bunge katika kuishauri na kuisimamia serikali kwa mujibu wa
madaraka ya bunge ya ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba ya sasa. Katika
muktadha huo, nimeanza kufanya uchambuzi ili kuwasilisha bungeni
mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni. Ukweli ni Uhuru!.
Hata hivyo, hata kwa kanuni zilizopo sasa udhaifu wa bunge unaongezeka
kutokana na maamuzi ya kizembe mathalani ya kutozingatia matakwa ya
kanuni za bunge, mfano Kanuni ya 94 inalitaka bunge ili kutekeleza
majukumu yaliyoainishwa katika ibara ya 63 (3) (c) ya Katiba kwa kukaa
kama kamati ya mipango katika mkutano wake wa mwezi Februari ili
kujadili na kushauri kuhusu mapendezo ya mpango wa taifa unaokusudiwa
kutekelezwa na serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata, kanuni ambayo toka
niingie bungeni haijawahi kutekelezwa kwa wakati hata mara moja pamoja
na kuwakumbusha wanaohusika kusimamia kanuni. Ukweli ni Uhuru!.
Mwaka huu udhaifu umekuwa mkubwa zaidi kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa
kwa mwaka wa fedha 2012/2013 sanjari na Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 tarehe 18 Juni 2012 na
kupitishwa siku moja tarehe 22 Juni 2012 hali ambayo imechangia katika
kufanya bajeti ya nchi isizingatie kwa ukamilfu mpango wa taifa wa miaka
mitano. Ukweli ni Uhuru!.
Nashukuru kwamba Spika wa Bunge Anna Makinda amekiri bungeni tarehe 20
Juni 2012 kwamba kulikuwa na udhaifu wa miaka mingi wa kutozingatia
kanuni ya 106 ambayo inalitaka bunge kujadili muswada wa sheria ya fedha
mwishoni baada ya bunge kukamilisha kazi ya kupitisha muswada wa fedha
za matumizi ili kuiwezesha serikali kuongeza vyanzo vya mapato kama
wabunge tulivyopendekeza mwaka 2011 na pendekezo hilo kurudiwa tena na
kamati ya fedha na uchumi tarehe 18 Juni 2012. Ukweli ni Uhuru!.
Izingatiwe kuwa iwapo sheria ya fedha ingepitishwa tarehe 22 Juni 2012
kama ilivyokuwa imepangwa awali athari zake zingekuwa kubwa kwa kuwa
udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu kubwa kwa Rais juu ya utaratibu wa
kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha kwa mujibu wa ibara ya 99 (1) kwa
kuweka masharti kwamba bunge halitashughulikia sehemu kubwa ya masuala
ya fedha isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo hilo
lishughulikiwe na bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa
kwenye bunge na waziri. Hivyo, michango na mapendekezo ya wabunge bila
Rais mwenyewe kupendekeza isingeliwezesha bunge kufanya mabadiliko ya
kupanua wigo wa mapato kwa kuwa kwa kuwa mujibu wa ibara 99 (2) (a) (i)
udhaifu wa bunge ni pamoja na kukatazwa kutoza kodi au kuongeza kodi.
Ukweli ni Uhuru!.
Hivyo, Kamati ya Fedha na Uchumi itumie vizuri mwanya wa ibara ya 99 (3)
kurejea maoni yake, ya kambi rasmi ya upinzani bungeni na michango ya
wabunge ya mkutano wanne wa Bunge mwaka 2011 na Mkutano wa nane wa Bunge
mwaka 2012 na kufanya marekebisho ya muswada wa sheria ya fedha kwa
kumshauri Waziri. Ukweli ni Uhuru!.
Aidha, ili kuondoa udhaifu uliopo Rais Kikwete mwenyewe asome kumbukumbu
rasmi za bunge (Hansard) za tarehe 18 Juni mpaka 22 Juni 2012 na
kuliongoza baraza la mawaziri kumwezesha Waziri wa Fedha ya 86 (10)
kuwasilisha muswada wa sheria uliochapishwa upya ukiwa na marekebisho au
mabadiliko yanayopaswa kufanyika yenye kulenga kupunguza kodi katika
bidhaa zenye kuchangia mfumuko wa bei na kupanua wigo wa mapato kwa
kuongeza kodi kwenye vyanzo mbadala tulivyovieleza bungeni. Ukweli ni
Uhuru!.
Izingatiwe kuwa nilipotolewa bungeni tarehe 19 Juni 2012 nilieleza kwa
ufupi nilichosema bungeni na nilichotarajia kusema na kuahidi kwamba
nitatoa tamko kamili baadaye; baada ya kujipa muda wa kutafakari
nimefikia uamuzi wa kutoa tamko husika wakati bunge litakapoelekea
kujadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio
ya mapato na matumizi ya ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2012/2013;
ambapo pamoja na masuala mengine nitaeleza hatua ambazo Rais anapaswa
kuchukua kuwezesha ahadi alizotoa kwa watanzania kuweza kutekelezwa na
serikali. Ukweli ni Uhuru!.
Kwa sasa niwashukuru wananchi wa Ubungo, wakazi wa mkoa wa Dar es salaam
na watanzania kwa ujumla walionielewa na kuniunga mkono kupitia maoni
yao kwenye mitandao ya kijamii, simu za mkononi na katika vyombo vya
habari. Nawashukuru pia viongozi wa dini, chama na asasi mbalimbali nje
na ndani ya serikali walionipa moyo wa kuendelea kusimamia ukweli na
kuacha unafiki ili kusimamia uwajibikaji wa viongozi kwa maendeleo ya
taifa. Ukweli ni Uhuru!.
Nashukuru pia kwa mchango wa walinipinga na kunikosoa kutokana na kauli
niliyotoa juu ya udhaifu wa Rais Kikwete, wapo walioeleza kuwa ilitokana
na jazba na wengine wameeleza kuwa ningetumia lugha ya diplomasia
kufikisha ujumbe ili kutodhalilisha taasisi ya urais na kwa kuzingatia
utamaduni wetu wa heshima kwa wakubwa na wapo wachache waliosema kwamba
ni matusi kutamka ‘udhaifu wa Rais’. Ukweli ni Uhuru!.
Wakati mjadala huu ukiendelea ni rai yangu kwamba rejea ifanyike katika
mchango wangu wa tarehe 5 Julai 2011 wakati wa mjadala wa makadirio ya
mapato na matumizi ya ofisi ya Rais kwa mwaka 2011/2012 na rejea kamili
pia ifanyike kwenye mchango wangu wa tarehe 19 Juni 201; na ieleweke
kwamba naheshimu taasisi ya urais na umri, naamini katika matumizi ya
lugha ya kidiplomasia, hata hivyo nilitafakari na kuamua kuusema ukweli
kwa lugha ya moja kwa moja ili ujumbe ufike kwa mamlaka zote
zinazohusika na wauchukulie kwa uzito tofauti ilivyokuwa mwaka mmoja
uliopita. Ukweli ni uhuru!.
Niliamini, naamini na nitaendelea kuamini kwamba kutamka neno ‘udhaifu
wa Rais’ sio kumtukana Rais na wala sio kulitumia jina la Rais kwa
dhihaka; hata hivyo kwa kuwa pamekuwepo na mwelekeo wa propaganda za
kudai kuwa kauli hiyo ni matusi na kwa kuwa chanzo cha propaganda hizo
ni udhaifu uliofanywa na Naibu Spika Job Ndugai bungeni wa kunihukumu
kwa kutumia kanuni tofauti na tuhuma iliyotolewa; nakusudia kukata rufaa
dhidi ya uamuzi wake ili kuwe na mjadala mpana wa kibunge utakaowezesha
kumbukumbu sahihi kuwekwa. Ukweli ni uhuru!.
Katiba ya Nchi ambayo niliapishwa kuilinda pamoja na ubovu wake inatamka
katika Ibara ya 63 (2) kwamba “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho
chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa
niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa
mujibu wa katiba”. Toka nichaguliwe kuwa mbunge mwaka 2010 kwa nyakati
na maeneo mbalimbali viongozi wa vyama, dini, asasi za kiraia, vyombo
vya habari na wananchi wa kawaida wakilalamika kuhusu udhaifu wa Rais na
kutaka atumie nguvu na mamlaka yake ya kikatiba kuiongoza kwa uthabiti
serikali kushughulikia masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii
yanayolikabili taifa; niliamua kuendelea kusema bungeni kwa mara
nyingine ikiwa ni sehemu ya kutimiza wajibu wa kibunge wa kuwakilisha
wananchi na kuisimamia serikali. Ukweli ni Uhuru!.
Tarehe 19 Juni 2012 nilieleza bungeni kabla ya kutolewa sababu za
kuikataa bajeti na tarehe 22 Juni 2012 nilipiga kura ya hapana ya
kuikataa bajeti kwa kutokuweka misingi thabiti ya kutimiza ahadi ya Rais
Kikwete na CCM ya maisha bora kwa kila mtanzania na badala yake
kuongeza ugumu wa maisha kutokana na kushindwa kukabiliana na matatizo
ya mfumuko wa bei. Aidha, kiwango cha fedha kwa ajili ya miradi ya
barabara na maji kwa upande wa jiji la Dar es salaam ikiwemo jimbo la
Ubungo ni kidogo tofauti na kile kilichotajwa na Rais Kikwete na
kuingizwa kwenye jedwali la Mpango wa Taifa wa miaka mitano kwa upande
wa miradi ya maendeleo iliyopaswa kutengewa fedha katika bajeti ya
2012/2013. Ukweli ni Uhuru!.
Pamoja na utetezi uliotolewa na Serikali juu ya mgongano kati ya tafsiri
kati ya kiingereza na Kiswahili, ukweli utaendelea kubaki kuwa tuliamua
kuikataa bajeti kwa kuwa ilishindwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa
Maendeleo wa Miaka Mitano ambao uliwasilishwa na Rais Kikwete na
ukapitishwa kwa azimio la bunge ambao ulipaswa kuiongoza serikali kuweka
mkazo katika kuendeleza nchi kwa kutumia fedha za ndani kwa kutenga
kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya maendeleo kama
zilivyokokotolewa katika mpango husika. Ukweli ni Uhuru!.
Naamini Rais Kikwete anayofursa ya kurekebisha udhaifu huo kwa kuongeza
nguvu zake katika muswada wa sheria ya fedha kupanua wigo wa mapato na
hatimaye kumwezesha Waziri wa Fedha kuwasilisha bungeni kwa mujibu wa
kanuni ya 107 mapendekezo ya matumizi ya nyongeza ya fedha za serikali
yenye kulenga kuongeza kiwango cha fedha za maendeleo. Kwa upande wa
Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam, serikali kwenye bajeti ya
nyongeza inayopaswa kuwasilishwa iongeze fedha za miradi ya Maji kwa
upande wa Ruvu Juu ikiwemo kutenga fedha za kutosha za ujenzi wa Bwawa
la Kidunda, kwa upande wa Barabara iongeze fedha za ujenzi kwa kiwango
cha lami kwa barabara za pembezoni za mchujo na za mzunguko za kupunguza
msongamano wa magari, na fidia ya ardhi kwa wananchi wa Kata ya Kwembe
wanaopaswa kuhama kupisha ujenzi wa Chuo Kikuu Muhimbili (MUHAS) Eneo la
Mloganzila. Ukweli ni Uhuru!.
Kwa Wasemaji wa CCM waliodai kwamba nimetoa lugha ya matusi dhidi ya
Rais na mwenyekiti wa chama chao wasome Kitabu cha Uongozi wetu na Hatma
ya Tanzania cha mmoja wa waasisi wa TANU na CCM Mwalimu Julius Nyerere
ambapo wakati huo taifa likiwa katika mtanziko alimueleza Rais wa
wakati huo kuwa ni ‘kiongozi dhaifu’ katika ukurasa wa 50 na kuendelea
kusema katika Ukurasa wa 51 na namnukuu “Kwa sababu ya
minong’ono-nong’ono ya watu wasiiona mbali kuhusu Rais, na kubabaishwa
anakobabaishwa na washauri wake wakuu, nililazimika kuiambia wazi wazi
Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kwamba najiona kuwa
ninao wajibu wa kumsaidia Rais amalize kipindi chake salama” . Ukweli ni
Uhuru!
Naamini Mwalimu Nyerere hakumtukana Rais Mwinyi, kwa hiyo kunituhumu
nimetukana ni kumtuhumu pia Marehemu Baba wa Taifa; narudia tena
kusisitiza kuwa udhaifu uliojitokeza ni kutokana na Rais kutokutumia kwa
uthabiti nguvu na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba ibara za 33, 34,
35, 36, 37, 38 na 99 juu ya utendaji wa serikali na utekelezaji wa
mipango mbalimbali ya maendeleo. Ukweli ni Uhuru!.
Nimalize kwa kunukuu kitabu kingine cha Mwalimu Nyerere cha miaka ya
mwanzoni mwa 1960 cha TUJISAHIHISHE, “ Makosa yetu mengine hutokana na
woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa, au
kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa.
Na msingi wa woga ni ubinafsi. Pengine huwa tunaogopa sisi wenyewe
kulaumiwa au kupata hasara fulani. Pengine twaweza kuwa hatuna cheo
chochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine huwa hatuna wala tamaa
yoyote ya kupata cheo fulani. Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya
kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii,
au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia
maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio
wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi
wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia.
Huu ni ubinafsi mbaya sana.", mwisho wa kunukuu: Ukweli ni uhuru.
Wenu katika utumishi wa umma,
John Mnyika
22 Juni 2012
Bungeni-Dodoma
No comments:
Post a Comment