Monday, June 11, 2012

NYAMA YA NGURUWE YAPIGWA MARUFUKU MJINI IRINGA, NI KWASABABU YA HOMA YA NGURUWe

Na Solomon Lekui

Picha hii ya maktaba yetu, inamuonesha Profesa Peter Msolla (Mbunge wa Jimbo la Kilolo) akiangalia jinsi wafanyabishara wa nyama ya nguruwe mjini hapa wanavyofanya biashara yao 
WAPENZI wa ile nyama ya nguruwe maarufu kama Kitimoto inayoaminika kuongeza kinga za mwili kwa watu walioshambuliwa na maambukizi ya Ukimwi kama utaila sana, imepigwa marufuku kuuzwa mjini Iringa kuanzia leo.

Hatua hiyo itakayowaacha mamia ya wafanyabiashara wake wakiathirika kiuchumi, imekuja baada ya ugonjwa wa homa ya nguruwe kuripotiwa kuingia mjini hapa.

Daktari wa Mifugo wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Augustino Nyenza amesema kuanzia leo machinjio zote za nguruwe zinatakiwa kufungwa kwasababu ya tatizo hilo.

Amesema tangu Mei 20 mpaka jana, ugonjwa huo ulikuwa umekwishauwa nguruwe 44 katika kata ya Mkwawa, huku uchunguzi uliofanywa ukioneshawa wengine wengi wanasumbuliwa na ugonjwa huo.

Alisema wakati halmashauri hiyo ikitangaza kuchinja na kuuza nyama ya nguruwe, wananchi wanatakiwa kusubiri karantini kubwa ya wilaya.

“Tunaendelea kufanya mawasiliano kuhusu hali ya ugonjwa mjini Iringa ili karantini iweze kutangazwa rasmi,” alisema.

Alisema karantini hiyo itazuia kuingiza, kutoa au kuuza nyama ya nguruwe mjini hapa mpaka pale itakapotangazwa vinginevyo baada ya ugonjwa huo kudhibitiwa.

Hii ni mara ya pili kwa ugonjwa huo wa nguruwe kuingia mjini hapa katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitatu iliyopita.

Mapema mwezi Machi mwaka jana, ugonjwa huo uliingia mkoani Iringa ukitokea mkoa jirani wa Mbeya ambako pia uliuwa idadi kubwa ya nguruwe.

Ugonjwa huo uliingia mkoani Mbeya ukitokea katika wilaya ya Kalonga nchini Malawi na baadae kuingia mkoani Iringa kwa kuanzia wilaya Ludewa ulikouwa nguruwe 145 kati ya 716 katika kijiji cha Lupingu na Ntumbali.

Baada ya kutangazwa kwa karantini, timu ya madaktari wa mifugo wa ofisi ya kanda na halmashauri ya manispaa ya Iringa na Iringa Vijijini waliwauwa kwa kuwachoma moto nguruwe 99 waliokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh Milioni 8.5, waliokamatwa wakisafirishwa kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam.

Katika tukio hilo lililokuwa la kusikitisha, nguruwe hao waliosafirishwa kwa kutumia gari la taka la manispaa ya Iringa na kupelekwa katika dampo la manispaa hiyo, walitumbukizwa wakiwa wazima kwenye shimo dogo lililokuwa na moto mkubwa uliowashwa kwa kutumia miti na matairi chakavu na baadaye kufa.

No comments:

Post a Comment